JINSI YA KUMLISHA MTOTO ALIYEZALIWA NA MAMA MWENYE VIRUSI VYA UKIMWI



Uambukizo wa virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto Kwa kawaida sio wanawake wote wenye virusi vya UKIMWI huwaambukiza watoto wao. Inakadiriwa kuwa kiasi cha asilimia 60 hadi 70 ya watoto wanaozaliwa na wanawake wenye virusi vya UKIMWI hawaambukizwi kabisa hata kama hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kupunguza uwezekano wa uambukizo Inakadiriwa asilimia 30 hadi 40 ya watoto huambukizwa virusi vya UKIMWI ambapo:
  • Asilimia 5 – 10 ya watoto wanaambukizwa wakati wa ujauzito
  • Asilimia 10 – 20 wanaambukizwa wakati wa uchungu na kujifungua
  • Asilimia 5 – 20 wanaambukizwa wakati wa kunyonyeshwa

Mambo yanayochangia kuongeza hatari ya uambukizo wa virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto:

  • Mama kuambukizwa virusi vya UKIMWI wakati wa ujauzito au wakati wa kunyonyesha. Wakati mama anapoambukizwa, huwa na virusi vingi mwilini kwa hiyo uwezekano wa kumwambukiza mtoto ni mkubwa zaidi.
  • Mama kuwa na UKIMWI. Uwezekano wa kumwambukiza mtoto ni mkubwa kwani mama atakuwa na virusi vya UKIMWI vingi mwilini mwake.
  • Mama kuwa na maambukizo ya magonjwa ya ngono wakati wa ujauzito. Magonjwa ya ngono husababisha michubuko ukeni ambayo huongeza hatari ya uambukizo wa virusi vya UKIMWI iwapo mama hafanyi ngono salama.
  • Taratibu zinazotumika wakati mama anapojifungua. Kwa mfano kuongeza njia ya uzazi, uchanaji mapema wa utandu, mtoto kunyonywa uchafu baada ya kuzaliwa.
  • Hali ya lishe ya mama. Mama mwenye hali nzuri ya lishe huwa na mfumo thabiti wa kinga ambao huchelewesha mama huyo kupata UKIMWI.
  • Hali ya matiti ya mama. Matiti yenye vidonda au michubuko, chuchu zinazotoa damu na majipu ya titi huongeza hatari ya mama kumwambukiza mtoto wake iwapo mtoto ananyonyeshwa.
  • Ulishaji wa kuchanganya maziwa ya mama na vinywaji au vyakula vingine. Vyakula na vinywaji kama maziwa mbadala, maji, chai, uji, maji ya matunda, n.k. huweza kusababisha michubuko kwenye utumbo wa mtoto na hivyo kutoa mwanya kwa uambukizo wa virusi vya UKIMWI.
  • Muda wa kunyonyesha. Kadiri kipindi cha kunyonyesha kinavyokuwa kirefu, ndivyo uwezekano wa kumwambukiza mtoto unavyoongezeka. Hatari huongezeka zaidi iwapo mama mwenye virusi vya UKIMWI atamnyonyesha mtoto wake kwa zaidi ya miezi sita kwani wakati huo mtoto hupewa vyakula vingine.
  • Hali ya kinywa cha mtoto. Vidonda vya kinywani au kooni na utandu mweupe kinywani kwa mtoto huweza kuongeza hatari ya uambukizo wa virusi vya UKIMWI kupitia sehemu hizo zenye vidonda.


“Ikumbukwe kuwa njia kuu ya kuzuia mtoto kupata virusi vya UKIMWI ni wazazi kuzuia wasiambukizwe virusi hivyo. Jukumu hilo ni la baba na mama.”

Kumlisha mtoto mchanga aliyezaliwa na mama mwenye virusi vya UKIMWI (miezi 6 ya mwanzo)

Tamko rasmi lililotolewa na mashirika ya kimataifa (WHO/UNAIDS/UNICEF)
linasisitiza mambo muhimu yafuatayo:
  • Mama mwenye virusi vya UKIMWI aelekezwe kikamilifu kuhusu hatari ya
  • kuambukizwa mtoto kupitia maziwa ya mama na njia nyingine;
  • Wanawake wahimizwe na wapewe huduma za ushauri nasaha na kupima virusi vya
  • UKIMWI kwa hiari (VCT);
  • Mwanamke mwenye virusi vya UKIMWI apewe taarifa muhimu na zilizo sahihi,
kumwezesha kufanya uamuzi sahihi wa njia ya kumlisha mtoto wake, iwe ni kunyonyesha kwa maziwa yake au kutumia maziwa mbadala.

KUMBUKA
Ni muhimu kuhakikisha kwamba wanawake ambao hawajaambukizwa virusi vya UKIMWI na wale wasiojua hali zao za uambukizo wanaendelea kushauriwa kunyonyesha maziwa yao, na wasishawishike kutumia maziwa mbadala kwa kuwaona wengine walioshauriwa na kuamua kutumia maziwa hayo.

Njia zinazoweza kutumika kumlisha mtoto mchanga tangu anapozaliwa mpaka miezi sita kwa mama anayeishi na virusi vya UKIMWI, Kumbuka kuwa katika miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto yeyote, maziwa ndiyo chakula pekee na muhimu sana. Maziwa hayo yanaweza kuwa ya mama au maziwa mengine. Ikiwa mtoto hanyonyeshwi maziwa ya mama basi apate maziwa mengine kiasi cha mililita (ml.) 150 za maziwa kwa kila kilo moja ya uzito wake kwa siku. Kwa mfano mtoto mchanga mwenye kilo tano anahitaji mililita (ml.) 750 za ujazo za maziwa (yaani ml. 150 x kilo 5) kwa siku, kiasi hiki kinaweza kugawanywa katika milo mitano au zaidi kwa siku. Ni muhimu kutumia kikombe kumlisha mtoto badala ya chupa ya kunyonya.

Hii hupunguza hatari ya maradhi ya kuhara kwani ni rahisi kusafishakikombe kuliko chupa.

Kuna njia kuu mbili zinazoweza kutumika kumlisha mtoto aliyezaliwa na mama mwenye virusi vya UKIMWI. Njia hizi ni kutumia maziwa ya mama na kutumia maziwa mbadala.

Kutumia maziwa ya mama
Mama aliyeamua kuchagua kutumia maziwa yake ana njia kuu tatu ambazo anaweza kuamua ni ipi itakayomfaa yeye na mtoto wake. Njia hizi ni:
  • Kunyonyesha maziwa ya mama pekee tangu mtoto anapozaliwa hadi miezi sita;
  • Kunyonyesha maziwa ya mama kwa muda mfupi (chini ya miezi sita);
  • Kutumia maziwa ya mama yaliyokamuliwa na kuchemshwa.
Kunyonyesha maziwa ya mama pekee tangu mtoto anapozaliwa hadi miezi 6
Tafiti zimeonyesha kuwa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee kunapunguza uwezekano wa mtoto kupata uambukizo wa virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama yake ukilinganisha na kumnyonyesha mtoto na wakati huo huo kumpa maziwa mengine, vinywaji au vyakula vingine. 

Iwapo mama atachagua njia hii anashauriwa:
Kumnyonyesha mtoto wake maziwa yake pekee kwa miezi sita ya mwanzo bila ya kumpa mtoto kitu kingine chochote hata maji. Kumpa mtoto maziwa mbadala, vinywaji au vyakula vingine huweza kuongeza hatari ya uambukizo wa virusi vya UKIMWI kwa mtoto. 

Vinywaji au vyakula hivyo huweza kusababisha michubuko Kwenye utumbo wa mtoto na hivyo kuruhusu virusi vya UKIMWI kupenya kwa urahisi;
  • Kuhakikisha mtoto ananyonyeshwa kila anapohitaji, usiku na mchana;
  • Kumpakata na kumweka mtoto vizuri kwenye titi ili kuzuia matatizo ya matiti yanayoweza kujitokeza, kama chuchu kupata mipasuko au michubuko. Matatizo hayo huongeza hatari ya uambukizo wa virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
  • Kuacha kabisa kumnyonyesha mtoto baada ya miezi sita. Wakati huo mama anaweza kukamua na kuchemsha maziwa yake akampa mtoto, huku akimpatia vinywaji na vyakula vingine.
Kunyonyesha maziwa ya mama kwa muda mfupi.
Kumwachisha mtoto kunyonya maziwa ya mama yake mapema husaidia kupunguza uwezekano wa mtoto kuambukizwa virusi vya UKIMWI kupitia maziwa. Kwa kufanya hivyo muda wa mtoto kuwa kwenye hatari ya uambukizo wa virusi vya UKIMWI hupungua.

Iwapo mama mwenye virusi vya UKIMWI atachagua njia hii anashauriwa kuacha kumnyonyesha mtoto wake mapema iwezekanavyo kabla ya miezi sita. Muda halisi wa kuacha kumnyonyesha mtoto utaamuliwa na mama mwenyewe kwa kuzingatia uwezekano wa kupata maziwa mbadala na uwezo wa kuyatumia ipasavyo.

Mama akumbuke kumnyonyesha mtoto maziwa yake pekee bila kumpa maziwa mbadala, vinywaji au vyakula vingine vyovyote. Uchanganyaji wa maziwa yanmama na maziwa mbadala, vinywaji au vyakula vingine huongeza hatari ya uambukizo wa virusi vya UKIMWI kwa mtoto. Mama anashauriwa kumpakata na kumweka mtoto vizuri kwenye titi ili kuzuia matatizo ya matiti yanayoweza kujitokeza.

Mama anapoamua kuacha kumnyonyesha mtoto wake ashauriwe kufanya hivyo katika muda mfupi. Ili kuweza kuzuia hatari ambazo zinaweza kujitokeza katika kipindi hicho cha mpito au kutokana na mabadiliko ya ghafla, mama ashauriwe kuanza kukamua maziwa yake katika wiki mbili kabla ya kumwachisha mtoto na kumnywesha mtoto maziwa hayo kwa kutumia kikombe. Hii itamwezesha mtoto kuweza kuzoea kutumia kikombe.

Mtoto aliyeachishwa kunyonya maziwa ya mama yake kabla ya miezi sita apewe maziwa mbadala au mama akamue maziwa yake na kuyachemsha kabla ya kumpa mtoto. Mtoto anyweshwe maziwa hayo mara tano au zaidi kwa siku, akizingatia kipimo cha mililita 150 kwa kila kilo ya uzito wake kwa siku.

Mama anayeamua kuacha kumnyonyesha mtoto wake mapema anapaswa kusaidiwa kufanya hivyo kwa ufanisi na usalama ili kuepusha madhara yoyote yanayoweza kutokea kwa mtoto.

Mama akiwa na hali mbaya, hasa anapopata magonjwa nyemelezi na akawa mgonjwa sana ni vyema aache kunyonyesha.

Kutumia maziwa ya mama yaliyokamuliwa na kuchemshwa.
Virusi vya UKIMWI vilivyoko kwenye maziwa ya mama vinaweza kuharibiwa kwa kuchemsha maziwa hayo yaliyokamuliwa. Tafiti zimeonyesha kuwa virusi hivyo hufa bila kuharibu kingamwili zilizopo kwenye maziwa iwapo yatapashwa moto kati ya nyuzi joto 56°C – 63°C kwa muda wa dakika 20. 

Lakini katika mazingira ya kawaida sio rahisi kupima nyuzi joto hizo hivyo inashauriwa kuacha maziwa hayo mpaka yachemke. Mara tu yakichemka yaipuliwe. Kwa kuchemsha maziwa hayo baadhi ya kingamwili na virutubishi vilivyomo hupungua. Ni muhimu mama apate ushauri wa daktari au mtaalamu wa afya kuhusu virutubishi vya nyongeza vya kumpa mtoto.

Iwapo mama ataamua kutumia maziwa yake aliyoyakamua na kuyachemsha yafuatayo ni muhimu.
  • Mama aelekezwe njia sahihi ya kukamua maziwa yake bila ya kusababisha maumivu ya titi lake;
  • Maziwa hayo yachemshwe na yaipuliwe pindi tu yanapoanza kuchemka;
  • Maziwa hayo yapoozwe kwa haraka aidha kwa kutumbukiza chombo chenye maziwa ndani ya maji baridi au kuweka ndani ya jokofu;
  • Mtoto anyweshwe maziwa hayo kwa kutumia kikombe;
  • Maziwa yachemshwe kiasi cha kutosha mlo mmoja tu. Maziwa yaliyochemshwa yasihifadhiwe kwa matumizi ya mlo unaofuata.
  • Mama anapochagua njia hii kama ilivyo kwa njia nyingine anapaswa kupata unasihi na kusaidiwa.


Kutumia maziwa mbadala
Maziwa mbadala yanaweza kutumika kumlisha mtoto aliyezaliwa na mama mwenye virusi vya UKIMWI. Maziwa mbadala ni pamoja na maziwa yaliyotengenezwa maalumu kwa watoto wachanga, maziwa yanayotayarishwa nyumbani kutokana na maziwa ya wanyama kama ng’ombe au mbuzi, maziwa ya unga yenye mafuta (dried full cream milk) au maziwa yaliyochevushwa (evaporated milk).

No comments

Theme images by hdoddema. Powered by Blogger.