AZAM FC YAZIDI KUIFUKUZIA SIMBA KIMYAKIMYA



ULIKUWA ni usiku mzuri kwa Azam FC, baada ya kuichapa Ndanda mabao 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 33 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) nyuma ya pointi mbili dhidi ya Simba iliyokileleni ambayo ina mchezo mmoja mkononi itakaoucheza kesho Jumapili na Ruvu Shooting.
Shukrani kwa mabao matatu ya nguvu yaliyofungwa na washambuliaji Yahya Zayd, Shaaban Idd na winga Enock Atta, yaliyoizamisha kabisa Ndanda, ambayo ilionyesha upinzani mkali katika mchezo huo.
Iliwachukua dakika ya 25 Azam FC kuweza kupata bao la uongozi, likifungwa na Zayd alipokea pasi safi ya Shaaban na kuwatoka mabeki wa Ndanda kabla ya kupiga shuti zuri nje kidogo ya eneo la 18 lililotinga wavuni.
Dakika tano baadaye Azam FC ilinufaika kwa mpira wa adhabu ndogo, baada ya winga Enock Atta kuitumia vema na kufunga bao la pili kwa mpira wa moja kwa moja uliomshinda kipa wa Ndanda, Jeremiah Kisubi.
Ndanda ilirejea mchezoni na kujipatia bao lake pekee lililofungwa na Nassor Kapama, kwa mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo uliomshinda kipa wa Azam FC, Razak Abalora na kufanya mpira huo uende mapumziko kwa wenyeji hao kuogoza 2-1.
Azam FC ilihitimisha ushindi wake kipindi cha pili baada ya Shaaban kuipatia bao la tatu akifunga kiustadi akiunganisha pasi safi ya juu ya winga Idd Kipagwile, ambaye naye alikuwa kwenye kiwango kizuri.
TPLB yaendelea kumsakama Kocha Azam FC
Katika mchezo huo, Azam FC ilimkosa kocha wake mkuu, Aristica Cioaba, ambaye alikuwa jukwaani baada ya kufungiwa na Bodi ya Ligi (TPLB) wakidai alionyesha ishara mbaya kwa mashabiki kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga.
Hii ni mara ya pili Bodi ya Ligi inamfungia kocha huyo, kifungo cha awali wakimuhusisha ametoa lugha chafu kwa waamuzi wakati wa mchezo wa Azam FC dhidi ya Ruvu Shooting.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea kuwepo kambini kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Simba utakaofanyika Uwanja wa Taifa Jumatano ijayo saa 10.00 jioni, ambapo kesho Jumapili itaanza programu kujiandaa na mechi hiyo.

No comments

Theme images by hdoddema. Powered by Blogger.