Ngoma shambulia kutokea kushoto, Chirwa simama kati, Ajib atokee kulia, tatizo kwa Mtibwa




NI ngumu sana Yanga SC kupoteza mechi ya ligi kuu Tanzania Bara ndiyo maana wanapotangulia kufungwa goli ‘hustuka’ haraka na kulikomboa. Hii ni sababu mojawapo ya kikosi kilicho na ubora wa kutosha na vipaji.
Katika michezo miwili ambayo wameangusha pointi msimu huu, mabingwa hao watetezi wa VPL walitangulia kuruhusu goli vs Lipuli FC siku ya ufunguzi wa msimu, lakini Donald Ngoma alisawazisha dakika mbili tu baadae.
Na namna walivyopambana hadi Mzimbabwe huyo (Ngoma) kusawazisha baada ya Majimaji FC  kuwatangulia kufunga katika uwanja wa Majimaji, Songea ni kielelezo halisi kuwa Yanga wana kikosi cha wachezaji waliopevuka kimchezo na wenye hitaji la kweli la mataji. Ndiyo maana hawapendi kupoteza mechi.
YANGA vs MTIBWA, Jumamosi hii
Licha ya kwamba kocha George Lwandamina bado ‘anahangaika’ kutengeza alama yake kiuchezaji katika kikosi cha Yanga, lakini ule ubora ambao tayari uliachwa na Mholland, Hans van der Pluijm utaendelea kuwasaidia
wakati mabingwa hao mara tatu mfululizo watakapowakabili vinara wa msimamo Mtibwa Sugar FC katika mchezo wa raundi ya tano msimu huu.
Mtibwa wameanza msimu kwa ushindi mara tatu na sare moja katika michezo minne. Kikosi hicho cha kocha Zubery Katwila kilifunga magoli manne katika michezo mitatu waliyocheza na kupata ushindi katika uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro, na goli lao la tano walifunga katika mchezo wanne na wa kwanza wakicheza ugenini  na
kulazimisha sare vs Ruvu Shooting wikendi iliyopita.
Wanakutana na Yanga huku wakionekana ‘kubezwa’ kwa safu yao ya mashambulizi ambayo imefunga magoli manne katika michezo minne iliyopita. Bado naamini Yanga wapo katika ‘umbo’ sahihi kiubora licha ya kutowafurahisha wapenzi wao kutokana na kiwango cha ‘wasiwasi’ katika michezo dhidi ya Lipuli, Njombe Mji FC, Majamaji FC, na Ndanda FC.
Ukweli Yanga  wamekusanya  alama  8  hapo  na  hilo  ni  jambo zuri  kwa  kikosi  kinachopitia mapito mengi ya kimabadiliko klabuni.
Katwila ambaye amepewa kibarua tangu Oktoba, 2016 akichukua nafasi iliyokuwa imeachwa na kocha wa sasa wa Taifa Stars, Salum Mayanga kikosi chake bado kitahitaji uzoefu mkubwa ili kuwazuia Ibrahim Ajib, Ngoma na Mzambia, Obrey Chirwa ambao wanataraji kuanza katika safu ya mashambulizi ya Yanga.
RAFAER DAUD



Kuendelea kujiamini na kuhimili presha ya kucheza katika timu kubwa kwa kiungo huyu mchezesha timu chipukizi ni mwanzo wa ‘kufufuka’ zaidi kiufungaji kwa kikosi cha Yanga. Ingawa bado Daud hajaonyesha ubora
wake wa moja kwa moja lakini kiwango chake vs Ndanda FC wiki iliyopita kilianza kumuangaza mchezaji ‘huyu wakati akiwa Mbeya City FC’ msimu uliopita.
Kitu ambacho Yanga wanaki-miss hivi sasa ni mchezaji ambaye ana uwezo wa kupiga pasi za mwisho, kuichezesha timu, kuichangamsha, kufunga magoli pale inapotokea na mwenye maarifa binafsi kimbinu na usomaji wa mchezo.
Daud anaweza kuendelea kuisaidia Yanga ikiwa ataongeza zaidi kiwango chake kutoka kile ambacho alikionyesha katika mchezo dhidi ya Ndanda.
Yanga inamuhitaji sana kwa wakati huu na yeye ndiye anayetegemewa kutambulisha mchezo wa Lwandamina ndani ya Yanga kama ambavyo Thabani Kamusoko alivyotambulisha mchezo wa Hans-kushambulia kwa kasi akitumia mipira mirefu.
Lwandamina anataka timu inayopasiana sana na kutegemea magoli yaliyotengenezwa kutokea katikati ya uwanja ndiyo maana timu yake haikimbizi katika wings.
NGOMA ASHAMBULIE KUTOKEA KUSHOTO
Ni kweli makocha huwa na mbinu  zao, lakini upande wangu bado sivutiwi na mbinu za mashambulizi katika kikosio cha Yanga hivi sasa.
Mara baada ya mchezo vs Ndanda ambao Ajib alifunga goli kali la mkwaju wa mbali, mbinu ya kumtumia Ngoma kama mshambulizi wa kati katika mfumo wa 4-3-3 sikuiafiki, ndiyo maana nilisema Lwandamina lazima akubali kumtumia Chirwa katika nafasi hiyo.
Si kwamba Ngoma hawezi majukumu hayo, hapana, ila kwa sasa ni magumu kwake kutokana na kupitia kipindi kigumu cha majeraha kwa miezi zaidi ya sita. Pia anapenda mchezo wa kukimbia.
Hans alipata magoli 17 kutoka kwa Ngoma na mengine 21 kutoka kwa Mrundi, Amis Tambwe wakati akiwacheza wawili hao kama washambuliaji-pacha msimu wa 2015/16. Na ilipotokea kutumia mfumo wa 4-3-3 alimtumia Ngoma kama mshambulizi wa tatu akishambulia kutokea upande wa kushoto.
Mabeki waliishia kumchezea faulo na Yanga ilipata zaidi ya mikwaju mitano ya penati baada ya Mzimbabwe huyo kuchezewa faulo na mabeki wa timu pinzani. Mtibwa ni ‘wahanga’ wa Ngoma wakati walipochapwa 2-0 Septemba, 2015 na kumalizwa kwa rekodi yao ya miaka 9 ya kutopoteza mechi vs Yanga katika ardhi ya Morogoro.
CHIRWA ACHEZESHWE KAMA MSHAMBULIZI WA KATI
Lwandamina aliwapanga, Chirwa, Ngoma na Ajib kwa mara ya kwanza vs Ndanda. Wote watatu hawakuonyesha uwezo mkubwa na hili lilitokana na kuwapanga vibaya licha ya kwanza alifanya machaguo mazuri ya kuanza katika safu yake ya washambuliaji watatu.
Wakati, Ngoma na Tambwe walipokutana na majeraha msimu uliopita, huku Malimi Busungu na Matheo Anthony wakishindwa kueleweka, Lwandamina aliamua kumpanga Chirwa kama kiongozi wa mashambulizi na Mzambia huyo aliwabeba hasa kutokana na nguvu zake, uwezo wake wa kumalizia mashambulizi, kumiliki mpira na chenga.
Katika mchezo uliopita alionekana kushindwa kuisaidia timu baada ya kupangwa upande wa kulia. Alikuwa anasimama muda mwingi na hakuonekana kuwa tayari kukimbilia mipira ya pembeni. Lwandamiana anaweza kufanikiwa zaidi ikiwa Chirwa atapangwa kati kwani mchezaji huyo anapenda kucheza hapo na Tambwe bado anajiandaa kurejea katika u-fiti baada ya majeraha ya muda mrefu.
AJIB A ASHAMBULIE KUTOKEA UPANDE WA KULIA
Safu ya mashambulizi ya Yanga itaanza kuwaziba midomo Jumamosi hii ikiwa kocha Lwandamina atawaanzisha tena washambuliaji wake watatu (Ngoma, Ajib na Chirwa) lakini ni hadi pale atakapowanga vizuri.
Kumpanga Ajib ashambulie akitokea upande wa kulia kutaongeza kasi na ubunifu katika mashambulizi ya Yanga. Wakati Chirwa hakuwa akitaka kubadilishana nafasi mara kwa mara, Ngoma na Ajib wanaweza kuwachanganya mabeki wa timu pinzani huku Chirwa akitengeneza nafasi na kusubiri pasi za mwisho.
Ajib ana ubunifu mkubwa, uwezo wa kukimbia na mpira, ana weza kushuti vizuri golini kwa timu pinzani, pia ni mpigaji mzuri wa pasi za
mwisho. Kama Lwandamina atawapanga vizuri washambuliaji wake hawa Yanga haitam-miss Papy Kabamba Tshishimbi ambaye atakosekana katika mchezo vs Mtibwa kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.




No comments

Theme images by hdoddema. Powered by Blogger.